25 Novemba 2023 - 14:28
Abu Ubaida atangaza baadhi ya hasara za Israel katika Kimbunga cha al Aqsa

Msemaji wa Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS), ametangaza kwamba zana na ala 335 za jeshi la Israel zimeharibiwa kabisa tangu kuanza mashambulizi ya utawala huo haramu dhidi ya watu wa Gaza na kusisitiza kuwa, utawala vamizi umelazimika kukubali suluhu na kusitisha mapigano.

Abu Ubaida amesema kwamba, yaliyokubaliwa katika mapatano hayo ndio kile kile ambacho wanamapambano wa Palestina walipendekeza kabla ya kuanza mashambulizi ya nchi kavu ya Israel na ambacho kilikataliwa na utawala huo haramu ukidai kwamba utafanikiwa kupata muradi wake kwa kutumia nguvu za kijeshi.

Msemaji wa Hamas amekariri kwamba njia pekee ya kuwarudisha mateka wa Israel ni kwa kubadilishana mateka, na kwamba Israeli haikupata chochote katika mashambulizi yake ya nchi kavu isipokuwa uharibifu, mauaji ya raia wa Palestina, kuua mateka wake zaidi, kurefusha mateso yao, na kupoteza idadi kubwa sana ya askari wake waliouawa na wengine kujeruhiwa kwenye uwanja wa vita.

Kuhusiana na makabiliano ya pande mbili, Abu Ubaida amesema wapigania uhuru wa Palestina wameharibu vifaru, mizinga, magari ya deraya na mabuldoza. Amesema wanamapambano wa Palestina wametekeleza makumi ya operesheni za aina yake zilizolenga wanajeshi wa Israel na kufanya mashambulizi ya makombora kwenye shabaha nyingi na masafa tofauti.Ameongeza kuwa, "Adui Mzayuni anaficha hasara yake halisi, ambayo tunaijua na tunaiona kwa macho, na askari wetu wanafuatilia kwa karibu na kuona mateso ya jeshi la Israel wakati wa kubeba maiti za askari wao walioangamizwa kutoka kwenye uwanja wa vita."

Msemaji wa Hamas amesema: Israel haina lengo katika kurefusha vita isipokuwa kufanya mauaji na uharibifu zaidi katika Ukanda wa Gaza.

Pia ametoa pongezi kwa harakati za Muqawama huko Yemen, Lebanon na Iraq na kusema: "Harakati hizo zinamzingira adui na kugonga ngome zake baada ya kuguswa na kilio cha Gaza na wito wa kuwatetea wakazi wake."

Usitishaji vita wa siku 4 huko Ukanda Gaza ulianza kutekelezwa jana Ijumaa katika siku ya 49 ya vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza.

Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yanajumuisha kuachiliwa huru mateka 50 wa Israeli kutoka Gaza ili kubadilishana na Wapalestina 150 kutoka kwenye magereza ya Israel, na kuingizwa Gaza mamia ya malori yenye misaada ya kibinadamu, vifaa vya matibabu na mafuta.



342/